Madereva wa magari ya aina ya Land Rover kutoka nchi mbalimbali wamekusanyika jijini Arusha, kaskazini mwa Tanzania katika tamasha maalum lenye lengo la kutangaza utalii pamoja na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa wa Arusha kwa kuwa na matukio mbalimbali yatakayokusanya idadi kubwa ya watu na hivyo kuchangia kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na la mkoa kwa Ujumla.
Tamasha hilo la siku tatu, limeanza Oktoba 12 na kutarajiwa kutamatika siku ya Jumatatu Oktoba 14, huku shughuli za tukio hilo zikianzia eno la Kingori nje kidogo ya jiji la Arusha kwa mkusanyiko mkubwa wa magari ambapo kila gari lilibandikwa namba yake ya ushiriki.
Msafara huo ulianza polepole ukikatiza maeneo mbalimbali ya jiji hilo ambapo wakazi walifurika kushuhudia. Kwa mujibu wa kitabu cha Guinness rekodi ya sasa ya dunia ya mkusanyiko wa magari mengi ya Land Rover ni ya mwaka 2018 ikishikiliwa na jimbo la Bavaria nchini Ujerumani ambapo magari 632 yalijitokeza na kutengeneza msafara uliofika umbali wa kilometa 7.4.