Takriban shilingi bilioni 2.57 zinatarajiwa kutumika katika halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ipo chini ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja TARURA – NGARA Eng. Christopher Masunzu alipokuwa akizungumza na Ishizwe TV.
Eng. Masunzu amesema fedha hizo zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 227 ambapo kilomita 1.4 itakuwa ni kiwango cha lami katika kata za kabanga na Ngara mjini huku kata nyinginezo sita zikinufaika na matengenezo hayo kwa kiwango cha changarawe.
Sanjari na hilo, TARURA wilaya ya Ngara inatarajia kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 20 ili kurahisisha shughuli za usafirishaji kwa wananchi ikiwemo kufika katika maeneo yasiyo fikika.