Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema idadi ya Watalii nchini imeongezeka hadi kufikia 5,360,247 sawa na 107.2% ya lengo la Watalii 5,000,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020.
Akitoa hotuba Bungeni Jijini Dodoma leo May 19,2025 kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Balozi Chana amesema “Idadi ya Watalii wa Kimataifa imeongezeka kwa 132.1% kutoka Watalii 922,692 mwaka 2021 hadi Watalii 2,141,895 mwaka 2024, idadi ya Watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa 307.9% kutoka Watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia Watali 3,218,352 mwaka 2024”
“Hatua hii imewezesha idadi ya Watalii kufikia 5,360,247 sawa na 107.2% ya lengo la Watalii 5,000,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020, ni rasmi sasa nilieleze Bunge lako tukufu kuwa kwa lengo la idadi ya Watalii lililowekwa na Ilani, tumetekeleza ikiwa ni mwaka mmoja kabla, hongera kwetu sote Tanzania”
“Kwa rekodi hizo pia Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), limeitaja Tanzania kuwa nchi iliyoongoza Afrika kwa mwaka 2024 kwa kuwa na ongezeko kubwa la Watalii ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19 ambapo utalii Tanzania ulikua kwa 48%, Ethiopia (40%), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%), haya ni matokeo yaliyochagizwa na maono na kujitoa kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika filamu za Tanzania: The Royal Tour na ile ya Amazing Tanzania”
