Jeshi la Israel lilitangaza Jumanne kuwa lilianzisha operesheni za ardhini kusini magharibi mwa Lebanon, kuashiria upanuzi wa uvamizi wake ambao maafisa wa Israel wamesema unalenga kuwarudisha nyuma wanamgambo wa Hezbollah kutoka mpakani.
Kama ilivyokuwa kwa operesheni zake za awali za ardhini nchini Lebanon zilizoanza Septemba 30, jeshi la Israeli lilielezea juhudi hizo mpya kama “operesheni ndogo, za ndani, zilizolengwa.” Kampeni hiyo ya ardhini inaambatana na mashambulizi makubwa ya angani, ambayo yamejumuisha mashambulizi ya anga kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut, pamoja na maeneo ya kusini na mashariki mwa Lebanon.
Jeshi la Israel lilisema Jumanne moja ya mashambulizi hayo ya anga yalimuua kamanda mkuu wa Hezbollah, Suhail Husseini, ambaye alihusika katika uhamisho wa silaha kutoka Iran hadi kwa kundi la wanamgambo lenye makao yake nchini Lebanon.