Chama cha Makamu wa Rais wa kwanza katika tifa la Sudan Kusini Riek Machar kimesema kuwa kinajaribu kumtafuta kiongozi huyo baada ya waziri wa ulinzi na mkuu wa usalama wa taifa hilo kuingia kwa nguvu katika makazi yake na kutoa hati ya kukamatwa.
Katika taarifa ya chama cha Machar cha SPLM-IO kimelaani ukiukaji wa wazi wa katiba na mkataba wa amani uliorekebishwa ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2013 hadi 2018 kati ya vikosi vinavyomtii Machar kwa upande mmoja na vile vya Rais Salva Kiir .
"Walinzi wake walinyang'anywa silaha na hati ya kukamatwa ilifikishwa ilitolewa kwa mashtaka ambayo hayakufahamika. Juhudi za kumhamisha kwa sasa zinafanywa," ilisema taarifa hiyo.
Serikali za kigeni zimeonya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kuzuka tena nchini Sudan Kusini kufuatia majuma kadhaa ya mvutano unaoongezeka ambao ulitokana na mapigano kati ya wanajeshi wa Serikali na wanamgambo ambao kihistoria wamekuwa karibu na vikosi vya Machar.
Katika kukabiliana na mapigano tangu mwishoni mwa mwezi Februari katika jimbo la Upper Nile kaskazini mashariki, serikali ya Kiir imewashikilia maafisa kadhaa wa chama cha Machar, akiwemo waziri wa mafuta ya petroli na naibu mkuu wa jeshi.