Shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) limetoa tahadhari juu ya kuongezeka kwa machafuko katika wilaya ya Walikale iliyopo jimbo la Kivu Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Shirika hilo limesema kuwa shughuli zake zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 wanaosaidiwa na jeshi la Rwanda.
Katika tangazo lake, shirika hilo lisilo la kiserikali la madaktari wasio na mipaka, MSF limetoa tahadhadhari kuhusiana na hatari inayotokana na uhaba wa dawa muhimu katika hospitali kuu ya Walikale, ikiwa mapigano yataendelea katika eneo hilo.
Tangu kuanza kwa mapigano kati ya kundi la wapiganaji wa M23 na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na vijana wazalendo, takribani asilimia 80 ya watu wameuhama mji huo huku wengine zaidi ya 700 wakiwa wamepatiwa hifadhi kwenye hospitali kuu ya Walikale ambayo inakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu kwa ajili ya wagonjwa.
Aidha, Shirika hilo limetoa wito wa kuimarishwa kwa usalama ili kuwezesha utoaji wa huduma za Afya kwa wahitaji, huku likihamasisha jamii na wadau wa kimataifa kuchukua hatua za haraka juu ya kinachoendelea.