Mapigano yamezuka kati ya waasi wa M23 na wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mapigano hayo mapya yalivunja makubaliano ya usitishwaji mapigano ambayo yalikuwa yamedumu kwa wiki kadhaa.
Duru za eneo hilo zimeeleza kuwa alfajiri ya jana Jumapili, waasi wa M23 walipambana na wanamgambo wakizalendo na kuwajeruhi raia 14 wakiwemo vijana wawili. Usitishaji mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ulianza mapema mwezi Agosti kufuatia upatanishi wa Angola.
Mazungumzo ya amani kati ya Kinshasa na Kigali yalikwama, lakini duru mpya ya mazungumzo imepangwa kufanyika mjini Luanda mwishoni mwa wiki ijayo. Rwanda inadai kuwa kuwepo kwa kundi la Wahutu wenye msimamo mkali wa FDLR eneo hilo, ni tishio kwa usalama wake.
Tangu M23 ilipoanzisha tena mashambulizi mwishoni mwa mwaka 2021, wameteka maeneo makubwa ya eneo hilo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini.