Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugu maji katika ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea katika maeneo hayo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Amesema magugu maji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.
Aidha, amewashukuru wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugu maji hayo.