Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kupitia Sehemu ya Sayansi ya Tiba na Maabara ya Wanyamapori imebainisha benki za sampuli za kibaolojia katika maabara, zinazosaidia kupata taarifa za uchunguzi wa kisayansi zinazotumika katika uhifadhi endelevu wa wanyamapori hapa nchini .
Akizungumza wakati wa zoezi la kuchakata na kuhifadhi sampuli hizo na taarifa zake, mtaalam wa maabara kutoka TAWIRI Anselmi Munga amesema, TAWIRI inajivunia kuwa na maabara za wanyamapori katika vituo vya Utafiti wa Wanyamapori Serengeti, Nyanda za juu Kusini na Makao Makuu ya Taasisi ambapo ndani yake kuna sampuli za kibaolojia za aina mbalimbali za wanyamapori zenye zaidi ya miaka 30.
“Benki hizi ni muhimu kwani hutunza sampuli za Kigenetiki, seli za kisomatiki, tishu, damu, na kuwa na datakanzu ya kisayansi ya wanayamapori wakiwemo waliokatika hatari ya kutoweka” amebainisha Munga.
Aidha, Munga ameeleza TAWIRI imeweka mkakati katika uhifadhi na utunzaji wa sampuli na taarifa zake kwa kuwezesha maabara kuwa na mfumo mzuri wa nishati ya umeme ambapo kuna majokofu yanayotumia umeme wa jua naumeme wa dharura (generator).
Pia sampuli zinahifadhiwa kwa kutumia mitungi ya kimiminika cha Naitrojeni na kemikali Munga Ameeleza, sampuli za wanyamapori zinatumika kusaidia katika mashtaka ya kijangili (forensic), kuandaa msingi wa utambuzi wa vinasaba (DNA) pamoja na kutoa taarifa za mabadiliko ya wanyamapori (evolution)
“kwa kutumia sampuli hizi tunaweza kubaini changamoto zinazokabili aina fulani ya wanyamapori kama vile magonjwa hivyo kuongeza jitihada za kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo ” ameeleza Munga