Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amemteua aliyekuwa meneja wa kampeni yake ya ushindi Susie Wiles, kuwa mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu ya Marekani (White House) na kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo yenye ushawishi.
Wiles anasifiwa sana ndani na nje ya watu wa karibu wa Trump kwa kuendesha kile ambacho kinaelezewa kuwa kampeni ya kimkakati wa hali ya juu na kufanya vyema. Tangu awali alionekana kuwa mshindani mkuu wa nafasi hiyo muhimu ya White House huku kwa kiasi kikubwa aliepuka kujitokeza hadharani hata kukataa kuzungumza wakati Rais mteule Trump alipokuwa akisherehekea ushindi wake Jumatano asubuhi.
Vilevile alikataa cheo rasmi cha meneja wa kampeni akikwepa kulengwa kutokana na historia ya Rais mteule Trump kwa watu waliochukuwa jukumu hilo.
Kuchaguliwa kwa Wiles ni uamuzi wa kwanza wa Trump na ambao unaweza kuelezea namna utawala wake ujao utakavyokuwa.