Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF, limeripoti kuwa zaidi ya wasichana milioni 370 na wanawake wadogo wanabakwa au kudhalilishwa kijinsia kote ulimwenguni kabla ya umri wa miaka 18. Takwimu hizo zimechapishwa katika makadirio ya kwanza ya kimataifa ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto kabla ya maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya msichana leo Ijumaa. Data hizi zina maana kwamba msichana mmoja kati ya nane ameathiriwa na aina hii ya unyanyasaji, mbali na unyanyasaji wa kijinsia wa mtandaoni au wa maneno, idadi ya wasichana na vijana wa kike walioathirika duniani kote wameongezeka hadi kufikia idadi ya takriban vijana milioni 650.