Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefanikisha uchukuaji wa taarifa za utafiti wa mafuta na gesi asilia katika eneo la nchi kavu la Bonde la Eyasi Wembere, Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania, likihusisha mikoa mitano ya Tabora, Singida, Arusha, Simiyu na Shinyanga. Awamu ya sasa ya utafiti imegusa mikoa mitatu: Singida (Mkalama na Iramba), Simiyu (Meatu), na Arusha (Karatu).
Meneja Mradi wa Utafiti wa Mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere, Mjiolojia Sindi Maduhu, ametoa taarifa hiyo katika kambi ya utafiti wa mafuta kijijini Bukundi, wilayani Meatu. Sindi amesema utafiti huu ulianza Agosti mwaka huu na umekusanya takwimu za mitetemo (2D Seismic Survey) zenye urefu wa kilomita 430, ambazo zimeonyesha maendeleo mazuri.
Sindi ameeleza kuwa utafiti huu ulihusisha zoezi la uthamini ambapo vijiji 15 katika mikoa hiyo vitapata fidia zikiwahusisha waathirika 541 kutokana na mazao yaliyoharibiwa wakati wa utafiti. Amehimiza wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo, ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, kwani shughuli za utafiti zimesitishwa kwa muda na zitaendelea kwenye Ziwa Eyasi mwezi Mei 2025.
Amesema TPDC pamoja na mkandarasi wake, AGS, wanafanya kazi ya kurejesha mazingira yaliyoathiriwa na mradi huo katika hali yake ya awali.
Sindi pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za utafiti wa mafuta na gesi asilia nchini. Ameishukuru pia Wizara ya Nishati, Bodi, na Menejimenti ya TPDC kwa usimamizi na mwongozo unaoleta tija katika shughuli za utafiti.