Waangalizi wa kimataifa kwenye uchaguzi wa Msumbiji wameelezea kuwepo kwa matukio kadhaa ya udanganyifu, huku vyama vya upinzani vikisema uchaguzi huo wa Jumatano uliofanyika katika hali ya amani, ulijaa wizi.
Katika taarifa yao ya hapo jana, waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema walishuhudia mabunda ya karatasi za kura zikiwa zimeshapigwa kwenye maeneo kumi tofauti, huku wasiwasi wa udanganyifu ukielezewa pia na taasisi ya IRI ya Marekani, ambayo waangalizi wake wamekosowa jinsi uchaguzi huo ulivyofanyika.
Kwa mujibu wa waangalizi hao, chama tawala cha Frelimo kilitumia vibaya rasilimali za nchi, wakiwemo wafanyakazi na vyombo vya usafiri vya umma, wakati wa kampeni kwenye majimbo yenye wafuasi wengi wa chama hicho na usajili wa wapigakura ukivuka asilimia 100.
Ingawa matokeo rasmi hayatazamiwi kupatikana kabla ya wiki mbili zijazo, lakini mgombea wa Frelimo, Daniel Chapo, anatarajiwa kushinda kwa wingi wa kura. Aidha, waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola wamezitaka mamlaka husika kuyashughulikia madai hayo ya udanganyifu ili kuzuia kadhia hiyo.