Baadhi ya wakulima wilayani Ngara mkoani Kagera wamenufaika na zoezi la ugawaji wa miche ya kahawa lililofanyika katika kitalu cha chivu kilichopo kata ya Ntobeye.
Wakizungumza na ISHIZWE TV wakulima hao wameeleza furaha yao baada ya kupokea miche hiyo huku wakiahidi kwenda kutekeleza zoezi la upandaji wa zao hilo kwa ufanisi lengo likiwa ni kufaidi matunda yake.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ntobeye Sande Mkozi, amesema kuwa miche hiyo inatolewa bure kwa wakulima wote waliojiorodhesha katika mashina yao huku akiwataka wakulima watakao nufaika na zoezi hilo kufuata taratibu na kanuni sahihi za upandaji wa zao la kahawa kwa ajili ya kapata manufaa maradufu.
Aidha, uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa miche ya kahawa katika halmashauri ya wilaya ya Ngara umeanza leo Oktoba 17, 2024 kwa kitaru cha Chivu chenye miche 100, 630 huku kata za Ntobeye, Kirushya na Murukulazo zikinufaika na zoezi hilo.