Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ametoa mwito kwa wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu ili kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika uchaguzi utakaofanyika nchini kote Novemba 27, 2024.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu mchakato wa uandikishaji wapigakura ulivyokwenda, Mchengerwa amesema fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hizo zitaanza kutolewa Oktoba 26, 2024 hadi Novemba 1, 2024. Waziri amevisisitiza vyama vya siasa kuhamasisha wananchama wao kujitokeza kwa wingi kusudi wananchi wawe na uwanja mpana wa kuchagua viongozi.
Aidha amewataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu watia nia wote wanahudumiwa kwa wakati pasipo changamoto zozote huku akibainisha tayari vyama vyote vimepata maelekezo sahihi kuhusu kuchukua na kurejesha fomu na hatua zingine za uchaguzi.