Mwenyekiti wa wafanyabiashara wilaya Ngara mkoani Kagera Crispin Medard Kamugisha ameiomba serikali kupitia mamlaka zinazohusika na biashara kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo wa kina wa kufanya shughuli zao.
Akizungumza na Ishizwe TV, Kamugisha ameeleza kuwa utolewaji wa elimu kwa wafanyabiashara hao ni jambo la msingi mno na linatakiwa kufanyika mara mara huku akisisitiza mfumo wa ukusanyaji kodi kwa wahusika kuwa rafiki kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta hiyo muhimu.
"Mimi kama mwenyekiti wa wafanybiashara wilaya ya Ngara nimekuwa nikizungumza na viongozi wa mamlaka husika juu ya umuhimu wa suala la elimu kwetu sisi, kwa sababu inasaidia namna ya kujua kufanya biashara kwa kutumia mifumo ya kidigitali pamoja na kuondoa kero zinazosababishwa na ukosefu wa elimu juu ya masuala ya biashara ikiwemo elimu ya mlipa kodi." anasema Kamugisha.
Aidha, Kamugisha ametoa rai kwa wafanyabishara wote wilayani humo kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari lengo likiwa ni kuirahisishia Serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii.