Askari Polisi ashinda Medali ya dhahabu

Askari Polisi ashinda Medali ya dhahabu

Mwanariadha wa Jeshi la Polisi Konstebo Transfora Mussa ameibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake kupitia mbio za kilometa 10 katika mbio za Fulham  zilizofanyika Nchini Uingereza Novemba 17, 2024 huku akifanikiwa kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa kwa kukimbia muda mfupi zaidi.

Mwanariadha huyo ambaye alipewa medali ya dhahabu, alivunja rekodi hiyo kwa kutumia muda wa dakika 31:53 tofauti na rekodi ya mwaka jana ambapo mwanariadha kutoka Nchini Kenya alishinda kwa kutumia muda wa dakika 33:11 katika mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya mwanariadha huyo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA), Mratibu Mwandamizi wa Polisi SSP Alphonce Bandya kwa niaba ya Kamanda wa Polisi pamoja na kumpongeza Mwanariadha huyo kwa kuliletea sifa Jeshi hilo, amesema wataendelea kutoa ushirikiano wakati wote kwa timu hiyo ili ipate mafanikio zaidi.

Kwa upande wake Konstebo Transfora mara baada ya kuwasili katika Uwanja huo wa ndege  Novemba 19, 2024 na kupokelewa na Maafisa, Wakaguzi na Askari amesema nidhamu pamoja maandalizi mazuri aliyoyafanya ndio msingi wa mafanikio hayo ambapo ameahidi kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine.

Kocha Msaidizi wa Timu hiyo Sajenti Oswald amesema usikivu na nidhamu wakati wa maandalizi katika kambi yao sambamba na kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi mzima wa Jeshi la Polisi pindi wanapouhitaji ndio chachu ya mafanikio yao.

Stars yalamba milioni 700  baada ya kufanikiwa kufuzu AFCON 2025

Stars yalamba milioni 700 baada ya kufanikiwa kufuzu AFCON 2025

Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwapa zawadi ya Tsh. milioni 700 Taifa Stars baada ya Tanzania kufuzu AFCON 2025 ambayo michezo yake itachezwa Morocco.

Akiongea na Wachezaji wa Stars Jijini Dar es aalaam  November 19,2024, Waziri Ndumbaro amesema “Rais Samia alikuwa kwenye mkutano Brazil lakini kila baada ya dakika Wasaidizi wake walikuwa wanampenyezea karatasi kumuonesha matokeo yakoje, karatasi ya kwanza ilisema Msuva amekosa goli, ya pili Feitoto kapaisha, ya tatu Mzize anawatapisha Mabeki, ya nne wakamwambia Msuva aliyekosa magoli kafunga bao, Mh. Rais anawapongeza sana, pili ameelekeza Bunge la February mualikwe Bungeni, tatu amesema leo amedondosha kwenu zawadi za pongezi Tsh. milioni 700 na Mama hana mbambamba”

Itakumbukwa Rais Samia pia alilipia tiketi zote za mchezo wa jana  na kuruhusu Wananchi kuangalia mchezo huo bure na pia alitoa ndege ya kupeleka timu ya Taifa CONGO DRC ambako Taifa Stars ilicheza na Ethiopia na kushinda mchezo huo.

Rodri ashinda tuzo ya Ballon d'Or kwa wanaume

Rodri ashinda tuzo ya Ballon d'Or kwa wanaume

Kiungo wa kati wa Manchester City na Uhispania Rodri ameshinda tuzo ya tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka (Ballon d'Or) kwa wanaume kwa mara ya kwanza. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alipoteza mchezo mmoja pekee msimu uliopita kwa klabu na taifa, alitunukiwa tuzo hiyo mjini Paris baada ya kuisaidia Uhispania kushinda Euro 2024 mwezi Julai huku akishinda Ligi Kuu, Uefa Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia akiwa na City.

Rodri, mchezaji wa kwanza katika historia ya klabu hiyo kushinda Ballon d'Or, alishinda tuzo hiyo mbele ya winga wa Real Madrid na Brazil Vinicius Jr. Tuzo ya Ballon d'Or inamtambua mwanasoka bora wa mwaka na hupigiwa kura na baraza la waandishi wa habari kutoka kila moja ya nchi 100 bora katika viwango vya ubora vya Fifa duniani kwa wanaume.

Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 2003 ambapo hakuna mshindi mara nane Lionel Messi, 37, au mshindi mara tano Cristiano Ronaldo, 39, kuonekana kwenye orodha ya walioteuliwa.Akiwa ameisaidia Manchester City kutwaa Treble (mataji Matatu} mwaka 2023, Rodri alimaliza wa tano katika tuzo ya Ballon d'Or mwaka jana.

Mafanikio yake yanayoendelea akiwa na City na nafasi yake ndani ya timu ya Uhispania iliyoshinda Euro 2024 imemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye ushawishi mkubwa katika soka la dunia. Mchezaji huyo wa kati alitoka nje akiwa ameumia wakati wa mapumziko katika mechi ya fainali ya Euro dhidi ya Uingereza, lakini alikuwa tayari amefanya ya kutosha kutangazwa mchezaji bora wa michuano hiyo.

Rodri alifunga mabao tisa bora zaidi kwa City msimu uliopita, ikijumuisha magoli mawili muhimu ya dakika za mwisho katika mechi za Ligi Kuu ya Uingereza na bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya West Ham.

“Leo marafiki wengi wameniandikia na kuniambia kuwa soka imeshinda, kwa kuwapa nafasi viungo wengi wa kati ambao wana kazi nyingi na leo inadhihirika,” anasema  Rodri ambaye alikabidhiwa tuzo hiyo ya  mwaka na mshindi wa mwaka 1995 George Weah.

"Mimi ni mvulana wa kawaida mwenye maadili, ambaye ninasoma, ambaye ninajaribu kufanya mambo sawa , na nimeweza kufika kileleni na ni shukrani kwenu nyote. " aliongeza Rodri

Aidha alipoulizwa kuhusu jeraha la mfupa wa paja ndani ya mfupa wa goti ambalo litamfanya awe nje kwa msimu huu, alisema kuwa  anajaribu tu kujitunza, kupumzika, kufurahia wakati wa mapumziko na familia yake  na  kluahidi kuwa atarudio akiawa nna nguvu  nguvu zaidi.

Yanga, Simba kuwania tuzo za CAF 2024.

Yanga, Simba kuwania tuzo za CAF 2024.

Miamba ya soka  Tanzania Simba na Yanga, imetajwa kuwania kipengele cha Klabu bora ya mwaka katika tuzo za shirikisho la soka  barani Afrika (CAF), zitakazotolewa Disemba 16 mwaka huu nchini Morroco.

Tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Disemba 16 mwaka huu, katika jiji la Marrakech Morroco, Klabu za Simba na Yanga zitachuana na Al Ahly, Mamelodi Sundows, Tp Mazembe, Petro Atletico, Zamalek, RS Berkane, Dream FC na Esperance de Tunis katika kipengele cha Klabu bora ya mwaka.

Yanga na Simba zilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali katika michuano ya klabu bingwa msimu uliopita, ambapo Klabu ya Yanga ilitolewa na Mabingwa wa Afrika kusini Mamelodi Sundows, wakati wekundu wa msimbazi waking’olewa na Mabingwa Al Ahly.

Kipengele kingine kilichotajwa ni mlinda lango bora wa mwaka ambapo golikipa wa Yanga Djigui Diarra anachauana vikali pamoja na golikipa wa Mamelodi Sundows Ronwen Williams, Andre Onana wa Manchester United na nyota wengine.

Paul Pogba kurejea tena  kwenye soka baada ya adhahabu yake kutamatika.

Paul Pogba kurejea tena kwenye soka baada ya adhahabu yake kutamatika.

Paul Pogba amedhamiria kurejea kwenye soka kufuatia kupigwa marufuku kujihusisha na mchezo huo baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli .

Nyota huyo wa Juventus alifungiwa  kwa miaka minne mwezi Februari baada ya kusimamishwa kwa muda na mahakama ya kitaifa ya Italia ya kupambana na dawa za kusisimua misuli (NADO Italia) Septemba mwaka jana.

Kufuatia kupigwa marufuku kwa muda, NADO Italia ilisema kuwa testosterone, ambayo inaweza kutumika kuongeza uvumilivu wa riadha, iligunduliwa kwenye mfumo wa kiungo huyo baada ya Juventus kuichapa Udinese 3-0,  huku Pogba akiwa  kwenye benchi kama mchezaji wa akiba ambaye hakutumika.

 Akizungumza na Sky Sports kiungo huyo alisem,a kuwa watu walifahamu,  na walipoona jambo hilo limetokea, walijua haikuwa makusudi “Mimi sio tapeli, mimi ni mtu ninayependa mchezo wangu na kupenda mchezo huo. Sipendi kudanganya, napenda kushinda kwa haki. Watu wanajua hilo. Mimi ni mpotevu mbaya lakini mimi si tapeli.” alisema kiungo huyo.

Pogba alifungiwa kucheza soka kwa miaka minne baada ya  kukutwa na hatia ya kutumia dawa iliyopigwa marufuku ya testosterone iliyogunduliwa kwenye mwili wake, hata hivyo adhabu hiyo ilipunguzwa   hadi miezi 18 na Mahakama ya Usuluhishi wa michezo ambapio nyota huyo anatarajia kurudi dimbani tena  ifikapo Machi 2025.

Visitor Counter

000833
Today: 3
Yesterday: 6
This Week: 41
Last Week: 60
This Month: 165

Opening Hours

  • Monday: 8.30am–6.30pm
  • Tuesday: 10.00am–8.00pm
  • Wednesday: 8.30am–6.30pm
  • Thursday: 8.30am–7.00pm
  • Friday: 8.30am–3.00pm
  • Saturday: 8.30am–2.00pm
  • Sunday: 8.30am–2.00pm

Contact Us

Kanani A Road, Mumasama Street,

P.O.BOX, 137

Ngara, Tanzania

Mobile:  +255 744 172 741

Email: info@ishizwemedia.co.tz